Tuesday, 9 August 2016







HISTORIA YA JIJI









Historia ya Halmashauri ya jiji la Arusha:

Historia inaonyesha kuwa mji wa Arusha ulianzishwa enzi za utawala wa Wajerumani katika mwaka 1890 ukiwa na eneo la 1.5 km2. Kati ya mwaka 1890 na 1906 mji uliendelea kupanuka, ni wakati huo huo ambapo uliojulikana kama miaka ya kuleta amani kwa sababu ya umuhimu wa sehemu hii kijeshi na kiserikali.

Wajerumani walijihakikishia kuwa wanatawala kwa ufanisi, hivyo walisisitiza dhana ya “Miaka ya Amani” sura ya mji hasa ilianza kujionyesha mwaka wa 1940 wakati wa utawala wa mwingereza. Mnamo mwaka 1948 mji wa Arusha ulipata hadhi ya kuwa mamlaka ya mji (Town authority) ukiwa na wakazi 5,320 tu.

Kwa upande mwingine, kufunguliwa kwa njia ya reli kutoka Tanga hadi Moshi mwaka 1912, kulisababisha kukua kwa mji wa Arusha kwa sababu ya kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi. Wagiriki waliokuja kwa kazi ya ujenzi wa reli, baada ya kumalizia reli hiyo wakawa wakulima wa katani na kahawa, aidha watu weusi (waafrika) nao walivutiwa na kuanzishwa kwa mji wa Arusha, kazi yao kubwa ilikuwa kilimo na ufugaji, eneo kubwa katika mji wa Arusha lilikuwa kwa ajili ya kilimo.

Mwaka 1900 Wajerumani walijenga boma na kituo cha kijeshi Mjini Arusha na kutawala eneo la mlima Meru. Karibu na boma yalianzishwa maduka ya wahindi, wagiriki na waarabu, walikuwa wanauza shanga, nguo, sabuni, mapambo, bakuli na sahani. Pamoja na maduka hayo yalikuwepo na mikahawa. Ukuaji wa mji uliendelea kujitokeza zaidi kati ya mwaka 1967 – 1978 kutokana na sababu zifuatazo:-
1. Kupanuka kwa mipaka ya Mji katika miaka ya 1967, 1972 na 1978
2. Arusha kuteuliwa kuwa makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
3. Arusha kuteuliwa kuwa miongoni mwa miji tisa ya kuendelezwa kuwa kitovu cha maendeleo ya viwandani Tanzania.

Mji ulipata hadhi ya kuwa Manispaa mwaka 1980, kufuatilia hali hii kumekuwepo na ongezeko la watu mjini uliosababishwa na uhamiaji kwa lengo la kujitafutia kazi kwenye viwanda, Ofisi mbalimbali, kufanya biashara na kuishi. Hali hii ilipelekea Serikali kuboresha huduma mbalimbali za kijamii na miundombinu kulingana na nafasi (hadhi ya Mji wa Arusha) kwa wakati huo. Kutokana na kupanuka kwa shughuli mbalimbali katika eneo la kilometa 93 tu za mraba, Serikali iliamua kupandisha hadhi ya Manispaa kuwa Jiji katika mwaka 2010 hivyo kutangaza eneo lake kutoka km2 93 hadi km2 208 (km2 115). Maeneo yaliyoongezwa yalikuwa ya Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.

Mawasiliano mazuri ya Jiji la Arusha na Mikoa ya Tanzania, nchi jirani na ulimwengu kwa ujumla, kwa njia ya barabara, anga reli na simu yameliweka Jiji katika mazizngira mazuri ya shughuli za kimaendeleo. Aidha eneo hili kufanywa kuwa mahakama ya kimataifa kwa ajili ya Rwanda, nako kumechangia kwa kiasi kikubwa kasi ya ukuaji wa Mji wa Arusha

No comments:

Post a Comment